Hashdu Shaabi kubuni mipango mipya ya kuwafukuza askari wa US Iraq
Harakati ya kujitolea wananchi ya Hashdu Shaabi ya Iraq imeonya kuwa, iwapo wanajeshi vamizi wa Marekani hawataheshimu uamuzi wa bunge la nchi hiyo wa kuwataka waondoke, basi itazindua mipango mipya ya kuwatimua askari hao katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Abu Ali al-Basri, Naibu Mkuu wa Vikosi vya Pamoja vya Hashdu Shaabi amesema askari vamizi wa Marekani lazima wafukuzwe nchini Iraq na kwamba harakati hiyo ya wananchi imepoteza wapiganaji wake wengi ili kuona azma hiyo inafanikiwa.
Al-Basri amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Al-Maalomah ambapo ameeleza bayana kuwa, uamuzi wa kuwatimua nchini humo wanajeshi wa Marekani ni wa wananchi wote wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Hashdu Shaabi amebainisha kuwa, katika hali ambayo Iraq inakabiliwa na changamoto nyingi, na wanasiasa wanatofautiana katika masuala mengi ya nchi, lakini karibu wote wanaafikiana kwa suala la kufukuzwa wanajeshi wa Marekani.
Mwezi uliopita pia, Falih al-Fayyaz, Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi ya Iraq alisisitiza ulazima wa kutekelezwa mpango uliopitishwa na bunge wa kutaka askari wa jeshi la Marekani waondoke nchini humo.
Askari wajeshi vamizi la Marekani wamepiga kambi nchini Iraq tangu mwaka 2003; na kambi yao kubwa kabisa ya kijeshi ya Ainul-Asad iko kwenye mkoa wa Al Anbar magharibi mwa nchi hiyo.
Wananchi wengi na makundi mbalimbali ya Wairaqi wanataka askari wa jeshi la kigaidi la Marekani waondoke nchini mwao; na bunge la Iraq pia lilipitisha mpango kuhusiana na kuondoka askari hao magaidi katika ardhi ya nchi hiyo mapema mwaka jana.