Makumi ya wanafunzi waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67328-makumi_ya_wanafunzi_waliotekwa_nyara_nigeria_waachiwa_huru
Huku vyombo vya usalama vya Nigeria vikiendelea kuwasaka wanafunzi wasichana zaidi ya 300 waliotekwa nyara na genge la watu waliokuwa na silaha mapema jana, makumi ya wanafunzi wengine waliotekwa wiki iliyopita wameachiwa huru.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2021 08:35 UTC
  • Makumi ya wanafunzi waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru

Huku vyombo vya usalama vya Nigeria vikiendelea kuwasaka wanafunzi wasichana zaidi ya 300 waliotekwa nyara na genge la watu waliokuwa na silaha mapema jana, makumi ya wanafunzi wengine waliotekwa wiki iliyopita wameachiwa huru.

Gavana wa jimbo la Niger, Abubakar Sani Bello amesema kuwa, watu 42 wakiwemo wanafunzi 27 waliotekwa nyara katika shule moja ya sekondari ya serikali katika wilaya ya Kagara jimboni Niger wiki iliyopita wameachiwa huru.

Watu hao wamepokewa na gavana huyo na wanatazamiwa baadaye kujumuika tena na jamaa zao. Haijabainika watu hao wakiwemo wanafunzi wameachiwa huru katika mazingira gani.

Kuachiwa huru makumi ya wanafunzi hao kumejiri siku moja baada ya majambazi waliokuwa na silaha Ijumaa asubuhi kuvamia shule moja ya sekondari ya wasichana katika jimbo la Zamfara nchini Nigeria na kuwateka nyara zaidi ya 300 miongoni mwao.

Genge la watu waliokuwa na silaha Jumatatu iliyopita liliwaachia huru mateka 53  wakiwemo wanawake na watoto liliowateka nyara kwenye basi nchini Nigeria siku chache nyuma.

Gaidi wa Boko Haram na wanafunzi wa shule ya upili ya Chibok; utekaji uliotikia dunia

Mbali na kushambuliwa shule hiyo ya sekondari ya wasichana na kutekwa nyara mamia ya wanafunzi, hivi karibuni pia kundi la kigaidi la Boko Haram liliwateka nyara wanafunzi wavulana 520 katika shule ya upili ya eneo la Kankara Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.

Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo anayekosolewa kwa kushindwa kudhibiti usalama na kukabiliana na magenge ya kigaidi na kijambazi amesisitiza kuwa, utekaji huo hautamshinikiza ajiuzulu.