Polisario yailaumu UN kwa mkwamo wa kisiasa Sahara Magharibi
Harakati ya Ukombozi ya Polisario inayopigania kuwa huru Sahara Magharibi imeulaumu Umoja wa Mataifa kwa mkwamo wa kisiasa katika mgogoro wa miongo kadhaa wa eneo hilo la kusini mwa Morocco.
Akizungumza jana Jumamosi katika kambi moja ya wakimbizi eneo la Sahara Magharibi, Brahim Ghali, kiongozi wa Polisario alisema: Tunaiomba UN itekeleze ahadi zake za kulikwamua eneo la Sahara Magharibi kutoka kwenye minyororo ya ukoloni, kwa mujibu wa hati na maazimio ya umoja huo.
Amesema watu wa jamii ya Saharawi wataendelea na mapambano yao ya ukombozi ili kulikomboa eneo la Sahara Magharibi na kuondokana na uwepo wa Wamorocco.
Harakati ya Polisario ni taasisi ya kisiasa na kijeshi ya wananchi wa eneo la Sahara Magharibi huko kaskazini magharibi mwa Afrika na kusini mwa nchi ya Morocco inayopigania kuwa huru eneo hilo.
Mgogoro wa Sahara Magharibi ulianza mwaka 1975 baada ya kufurushwa wakoloni wa Uhispania katika eneo hilo.
Morocco ililiteka eneo hilo, lakini harakati ya Polisario ambayo iliundwa mwaka 1973 ili kupambana na wakoloni wa Uhispania inasema kuwa Sahara Magharibi ni nchi huru inayokaliwa kwa mabavu na Morocco.