DRC: Chanjo milioni 1.7 za Covid 19 za AstraZeneca zawasili nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67466-drc_chanjo_milioni_1.7_za_covid_19_za_astrazeneca_zawasili_nchini
Zaidi ya dozi milioni moja na laki saba za chanjo ya Covid-19 zilizotengenezwa na Kampuni ya AstraZeneca jana Jumanne zilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa N'djili huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia mpango wa COVAX.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 03, 2021 04:40 UTC
  • DRC: Chanjo milioni 1.7 za  Covid 19 za AstraZeneca zawasili nchini

Zaidi ya dozi milioni moja na laki saba za chanjo ya Covid-19 zilizotengenezwa na Kampuni ya AstraZeneca jana Jumanne zilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa N'djili huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia mpango wa COVAX.

Mpango huo wa utoaji chanjo wa COVAX duniani unajumuisha taasisi kama muungano kwa jina la Coalition for Epidemic Preparedness Innovations (CEPI) , the Vaccine Alliance, Unicef na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Chanjo hizo za Covid-19 zilizowasili jana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni sehemu ya kwanza ya usambazaji wa chanjo dhidi ya corona ambao utaendelea kwa wiki kadhaa zijazo nchini humo. Mamlaka husika nchini Kongo zimeamua kutumia chanjo iliyotengenezwa na Kampuni ya AstraZeneca kwa sababu inaendana na mazingira ya kuzihifadhi chanjo hizo ya nyuzi joto kati ya 2 na 8. 

Eteni Longondo Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye amepokea shehena hiyo ya chanjo ya Covid-19 ya AsraZeneca amesema kuwa, hiyo ni hatua ya kihistoria kuelekea kuhakikisha chanjo dhidi ya maradhi ya corona zinagawiwa kwa usawa duniani kote. Amesema dozi hizo za chanjo milioni moja na laki saba walizopokea ni sehemu ya ugawaji mkubwa wa chanjo kuwahi kufanywa katika historia nchini humo.  

Eteni Longondo, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo