Magaidi washambulia tena raia nchini Nigeria, 6 wauawa
Raia wasiopungua 6 wameuawa katika shambulio jipya la watu wenye silaha katika mji wa Dikwa wa kaskaini mashariki mwa Nigeria
Taasisi na asasi kadhaa za kiraia jana Jumatano zilitangaza kuwa, watu wasiopungua 6 wameuawa katika mashambulizi ya Jumatatu na Jumanne wiki hii na wengine wengi wamejeruhiwa.
Baada ya kuenea taarifa hizo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mashambulizi hayo yamefanywa na magenge ya watu wenye mfungamano na Daesh (ISIS) ambao wameshambulia mawakala kadhaa wa misaada ya kibinadamu pamoja na kuchoma moto hospitali moja.
Takwimu za Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, mashambulizi ya kigaidi ya miaka 10 iliyopita yanayofanywa na genge la Boko Haram huko Nigeria yameshaua zaidi ya watu 30 elfu na kuwakosesha makazi karibu watu milioni 3.
Tangu mwaka 2009 hadi hivi sasa, jinai za genge la Boko Haram ambalo linadai kuwa elimu na masomo ya Magharibi ni haramu, zimeshasababisha hasara kubwa sana ndani na nje ya Nigeria.
Mwaka 2015 genge hilo la ukufurishaji lilipanua wigo wa jinai na mashambulizi yake hadi katika nchi za Niger, Cameroon na Chad.
Baada ya kuingia madarakani rais wa hivi sasa wa Nigeria, Muhammadu Buhari alizitembelea nchi hizo tatu zinazopakana na nchi yake na kutangaza kuundwa kikosi cha pamoja cha kukabiliana na Boko Haram, lakini hakuna matunda yoyote yaliyopatikana ya kuundwa kikosi hicho. Kila kukicha magaidi wa Boko Haram wanaendeleza jinai zao dhidi ya watu wasio na hatia.