Wanafunzi karibu 30 watekwanyara kaskazini magharibi mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67816-wanafunzi_karibu_30_watekwanyara_kaskazini_magharibi_mwa_nigeria
Afisa mmoja wa usalama nchini Nigeria ameripoti kuwa, wanafunzi karibu 30 wametekwanyara katika jimbo la Kaduna huko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2021 23:05 UTC
  • Wanafunzi karibu 30 watekwanyara kaskazini magharibi mwa Nigeria

Afisa mmoja wa usalama nchini Nigeria ameripoti kuwa, wanafunzi karibu 30 wametekwanyara katika jimbo la Kaduna huko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Kamishna wa Usalama wa jimbo la Kaduna huko Nigeria jana Ijumaa alitangaza kuwa, wanafunzi karibu 30 wa kike na kiume wametoweka na hadi sasa hajulikani walipo baada ya watu wenye silaha kukishambulia chuo jimboni humo. Afisa huyo wa usalama ameongeza kuwa, jeshi la Nigeria limefanikiwa kuwanusuru wanafunzi 180 chuoni hapo baada ya kujiri utekaji nyara huo. 

Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na tukio hilo la utekaji nyara hata hivyo karibu miezi miwili iliyopita wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram liliwateka nyara zaidi ya wanafunzi wa kiume 300 katika jimbo la Katsina huko Nigeria. 

Matukio ya utekaji nyara wanafunzi yamekithiri huko Nigeria ambapo mwezi Aprili mwaka 2014 magaidi wa kundi la Boko Haram liliwateka nyara wanafunzi mabinti 276 walioko hosteli shuleni kwao katika eneo la Chibok, kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.

Wanafunzi wa Chibok walipotekwa nyara na Boko Haram mwaka 2014 

Wanafunzi karibu 100 hawajapatikana hadi sasa.  Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lenye makao yake huko Nigeria lilianza kufanya mashambulizi na jinai mbalimbali nchini humo kuanzia mwaka 2009; na kisha kuanzia mwaka 2015 kundi hilo likaanza kuendesha mashambulizi katika nchi za Niger, Chad na Cameroon.