Mgombea wa urais Congo Brazaville aaga dunia kwa Covid-19
(last modified Mon, 22 Mar 2021 11:02:00 GMT )
Mar 22, 2021 11:02 UTC
  • Mgombea wa urais Congo Brazaville aaga dunia kwa Covid-19

Mgombea wa urais aliyetazamiwa kumpa ushindani mkubwa Rais Denis Sassou Nguesso katika uchaguzi wa rais wa jana katika Jamhuri ya Congo Brazaville ameaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19.

Guy Brice Parfait Kolelas, kinara wa chama cha upinzani cha Union of Humanists Democrats mwenye umri wa miaka 61 amefariki dunia akipelekewa nchini Ufaransa kwa ajili ya matibabu.

Hayo yamethibitishwa na Christian Cyr Rodrigue Mayanda, Mkurugenzi wa Kampeni za mwanasiasa huyo wa upinzani nchini Congo Brazaville ambaye amesema: "Kolelas aliaga dunia jana alasiri akiwa ndani ya ndege akielekea Ufaransa."

Hapo jana, familia yake ilisema kuwa mwanasiasa huyo wa upinzani amelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Inaarifiwa kuwa, kiongozi huyo ambaye pia alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari aligunduliwa kuambukizwa virusi vya Corona baada ya kufanyiwa vipimo Ijumaa iliyopita.

Rais Sassou Nguesso wa C. Brazaville

Ikumbukwe kuwa, mwanasiasa huyo ambaye ni mtoto wa kiume wa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Bernard Kolelas, aliibuka wa pili katika uchaguzi tata uliogubikwa na ghasia wa mwaka 2016.

Rais Denis Sassou Nguesso (77) ambaye ameiongoza nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kwa miaka 36 anatazamiwa kuibuka mshindi kwa muhula wa nne katika uchaguzi huo. 

 

 

Tags