Milio mikubwa ya risasi yasikika karibu na ofisi ya rais nchini Niger
Milio mikubwa ya risasi imesikika mapema leo karibu na ofisi ya rais wa Niger katika mji mkuu wa nchi hiyo Niamey, siku mbili kabla ya kuapishwa rais mpya Mohamed Bazoum.
Mashirika ya habari yameripoti kuwa, milio mikubwa ya risasi ilisikika kuanzia saa tisa alfajiri na kuendelea kwa muda wa nusu saa mjini Niamey.
Serikali ya Niger haijatoa maelezo yoyote kuhusu tukio hilo.
Mashambulio ya makundi yanayobeba silaha pamoja na mivutano ya kisiasa imeongezeka nchini Niger tangu Bazoum aliposhinda urais katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi Februari. Aliyewahi kuwa rais wa nchi hiyo Mahamane Ousmane, ambaye alishindwa katika kinyang'anyiro hicho ameyakataa matokeo hayo akidai kwamba ulifanyika udanganyifu.
Wiki iliyopita, mahakama ya juu ya Niger ilithibitisha ushindi wa Mohamed Bazoum na kuruhusu mgombea huyo wa chama tawala kuapishwa katika hafla iliyopangwa kufanyika siku ya Ijumaa.
Kutawazwa kwa Bazoum, litakuwa tukio la kwanza la mapokezano ya madaraka baina ya viongozi wawili waliochaguliwa kidemokrasia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Mohamed Bazoum, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya ndani wa Niger amefadhilishwa kuwa mrithi wa Rais Mahamadou Issoufou aliyeng'atuka madarakani baada ya kumalizika mihula yake miwili ya vipindi vya miaka mitano.../