23 wauawa katika mauaji mengine ya halaiki Mashariki mwa Congo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i68530-23_wauawa_katika_mauaji_mengine_ya_halaiki_mashariki_mwa_congo_dr
Afisa mmoja wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa watu waliokuwa na silaha ambao wanadhaniwa kuwa ni wapiganaji wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda wameua raia wasiopungua 23 huko Mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Apr 01, 2021 03:02 UTC
  • Waasi wa ADF
    Waasi wa ADF

Afisa mmoja wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa watu waliokuwa na silaha ambao wanadhaniwa kuwa ni wapiganaji wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda wameua raia wasiopungua 23 huko Mashariki mwa nchi hiyo.

Gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini, Carly Nzanzu Kasivita amewaambia waandishi habari kwamba, waasi hao wameshambulia kijiji cha Beu Manyama-Moliso katika eneo la Beni na kuua raia wasiopungua 23 katika mauaji mengine ya halaiki kwenye eneo hilo. 

Ofisi ya Gavana Carly Nzanzu ilisema Jumatano ya jana kwamba idadi ya vifo iliyotajwa ilikuwa ya awali wakati utafutaji wa miili ya wahanga wengine wa ukatili huo ukiendelea. Wapiganaji wawili wa kundi hilo la uhalifu pia wameuawa baada ya jeshi la Congo kuingilia kati.

Mnamo Machi 19, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, kundi la ADF limezidisha mashambulizi yake huko Mashariki mwa Congo DR na kwamba, tangu mwanzoni mwa mwaka huu limeuwa karibu watu 200 na kuwalazimisha wengine 40,000 kukimbia makazi yao.

Waelfu ya raia wa Mashariki mwa Congo DR wamelazimika kukimbia makazi yao.

Mwaka jana, UN ilisema mashambulizi ya kundi hilo yanaweza kutambuliwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu na jinai ya kivita.