Apr 01, 2021 10:40 UTC
  • AU: Hatua za dharura zichukuliwe kuinusuru Msumbiji

Umoja wa Afrika (AU) umetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za dharura katika ngazi za kieneo na kimataifa kufuatia kushtadi harakati na mashambulio ya magenge ya kigaidi kaskazini mwa Msumbiji.

Katika taarifa iliyotolewa leo Alkhamisi, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika sambamba na kulaani mashambulio ya kigaidi ya hivi karibuni yaliyoua makumi ya watu kaskazini mwa Msumbiji, ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kudhibiti hali katika mji wa pwani wa Palma, uliotekwa na magaidi Machi 24.

Amesema AU inatiwa wasiwasi mkubwa na ripoti za kuwepo kwa magenge ya kimataifa yenye misimamo ya kufurutu ada kusini mwa bara Afrika.

Mbali na makumi ya watu kuuawa, wengine zaidi ya 8,000 wamefurushwa au wamelazimika kuyahama makazi katika mji huo ulioko mkoani Cabo Delgado, kufuatia hujuma hiyo ya Jumatano ya wiki iliyopita.

Wakati huohuo, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) jana Jumatano ilifanya mkutano wa dharura mjini Harare, Zimbabwe kujadili hali ya mambo Msumbiji. Hata hivyo hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu hatua zitakazochukuliwa na jumuiya hiyo ya kieneo kunusuru hali ya Msumbiji.

Magaidi wa ISIS mjini Palma, Msumbiji

Haya yanajiri huku Wizara ya Ulinzi ya Msumbiji ikitangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeanzisha oparesheni kubwa ya kukomboa mji huo wa pwani wa Palma unaodhibitiwa na kundi linalojiita al-Shabaab.

Genge la kigaidi la ISIS limetangaza pia kuhusika na shambulio hilo la kuuteka mji huo wa Pwani kaskazini mwa Msumbiji, wenye akiba kubwa ya gesi inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 20.

Tags