Makumi ya wahajiri wafa maji katika pwani ya Djibouti
(last modified Tue, 13 Apr 2021 07:00:13 GMT )
Apr 13, 2021 07:00 UTC
  • Makumi ya wahajiri wafa maji katika pwani ya Djibouti

Wahajiri wasiopungua 34 wamepoteza maisha katika ajali ya boti iliyotokea katika mji wa bandari wa Obock, katika pwani ya Djibouti.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM), wahajiri hao walipoteza maisha alfajiri ya jana baada ya boti yao iliyokuwa imebeba abiria 60 kuzama ikitokea Yemen.

Mohammed Abdiker, Mkurugenzi wa IOM katika kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika amesema wahajiri hao walikuwa wakisafirishwa na wafanya magendo ya kinadamu.

Afisa huyo wa IOM amebainisha kuwa, miili ya watoto wengi sana imeopolewa majini baada ya kujiri ajali hiyo katika pwani ya Djibouti.

Mapema mwezi uliopita wa Machi, wahajiri zaidi ya 20 walipoteza maisha baada ya kugharikishwa majini na wafanya magendo, wakiwa katika boti iliyokuwa imejaa kupindukia ikilekea nchini Yemen kutoka Djibouti, mashariki mwa Afrika.

Wahajiri wa Kiafrika katika safari hatarishi ya baharini

Wahamiaji haramu raia wa Somalia na Ethiopia wamekuwa wakiaga dunia katika ajali hatarishi za namna hii za kujaribu kwenda Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, wakikimbia makali ya njaa, umaskini na vita katika nchi zao.

Oktoba mwaka jana 2020, wahajiri wanane wa Kiafrika waliaga dunia baada ya wafanya magendo kuwalazimisha kuondoka kwenye boti na kuruka majini karibu na Djibouti.