Taharuki yatanda Somalia, risasi zarindima Mogadishu; makazi ya rais wa zamani yashambuliwa
Hali ya taharuki imetanda nchini Somalia huku milio ya risasi ikirindima katika mji mkuu Mogadishu, baada ya maafisa usalama kukabiliana vikali na 'waasi' wanaopinga kurefushwa muda wa uongozi wa Rais wa nchi hiyo, Mohamed Abdullahi Farmaajo.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Somalia, Hassan Hundubey Jimale ametoa mkono wa pole kwa wahanga wa machafuko hayo ya jana Jumapili, ingwaje hajasema idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa.
Amesema watu fulani ambao hawajali chochote kuhusu usalama wa taifa hilo walianzisha hujuma hiyo, lakini anasisitiza kuwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika vimewarejesha nyuma.
Kadhalika amekanusha madai kuwa maafisa usalama ndio waliovamia makazi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Hassan Sheikh Mohamud katika eneo la Marino. Mohamud ambaye kwa sasa ni kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Somalia amesema Rais Farmaajo anapaswa kubebeshwa dhima kwa hali inayoshuhudiwa hivi sasa nchini humo na kwa 'kuagiza' wanajeshi washambulie makazi yake.
Kadhalika kiongozi mwingine mashuhuri wa upinzani nchini humo, Abdirahman Warsame amedai kuwa wanajeshi wa serikali wamevamia makazi yake pia viungani mwa Mogadishu.
Hivi karibuni, Rais Farmaajo alitia saini sheria ya kuongeza muda wa kukaa madarakani kwa miaka miwili, baada ya Bunge la nchi hiyo kupasisha muswada wa sheria hiyo Aprili 12. Wabunge nchini Somalia walipasisha muswada huo baada ya serikali ya Rais Farmaajo kushindwa kuandaa uchaguzi mwezi Februari mwaka huu baada ya muda wake kumalizika.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetangaza kuwa, liko tayari kuandaa na kusimamia mazungumzo ya kukwamua mgogoro huo wa kisiasa unaoikabili Somalia.