Kadhaa wauawa katika maandamano ya kushinikiza utawala wa kiraia Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69508-kadhaa_wauawa_katika_maandamano_ya_kushinikiza_utawala_wa_kiraia_chad
Kwa akali watu wawili wameuawa huku wengine 27 wakijeruhiwa katika maandamano ya ghasia yaliyozuka nchini Chad, kushinikiza utawala wa kiraia. Baraza la Kijeshi lilitangaza kuchukua hatamu za uongozi wa nchi kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Idriss Deby. 
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 27, 2021 13:07 UTC
  • Kadhaa wauawa katika maandamano ya kushinikiza utawala wa kiraia Chad

Kwa akali watu wawili wameuawa huku wengine 27 wakijeruhiwa katika maandamano ya ghasia yaliyozuka nchini Chad, kushinikiza utawala wa kiraia. Baraza la Kijeshi lilitangaza kuchukua hatamu za uongozi wa nchi kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Idriss Deby. 

Youssouf Tom, Mwendesha Mashtaka Mkuu katika mji mkuu N'Djamena amesema mwanamke mmoja ameuawa leo Jumanne baada ya askari wa kupambana na ghasia kushambulia basi katika wilaya ya Dembe huku mwanamme mmoja akiuawa katika maandamano ya ghasia kusini mwa nchi.

Maandamano hayo yanafanyika licha ya Albert Pahimi Padacke kuteuliwa na baraza hilo la kijeshi linaloongozwa na Mahamat Idriss Deby, mwana wa kiume wa hayati Deby, kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Chad anatazamiwa kuongoza serikali ya mpito ya Chad kwa muda wa miezi 18 kabla ya kuitishwa uchaguzi mwingine.

Deby katika enzi zake na maafisa wa jeshi la nchi hiyo

Deby ambaye alikuwa ameiongoza Chad kwa kipindi cha miaka 30, aliuawa hivi karibuni kabla ya kuapishwa kuiongoza nchi hiyo kwa awamu ya sita baada ya Kamisheni ya Uchaguzi kumtangaza mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 11 mwezi huu wa Aprili.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetoa taarifa likielezea wasiwasi lilionao kuhusiana na hali ya mambo huko nchini Chad, likisisitiza kuwa, kuna haja ya kurejeshwa utawala wa kiraia nchini humo na kuheshimiwa katiba ya nchi.