AU yamteua rais wa zamani wa Ghana kuwa mjumbe wake Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69912-au_yamteua_rais_wa_zamani_wa_ghana_kuwa_mjumbe_wake_somalia
Umoja wa Afrika umemteua aliyekuwa rais wa Ghana, John Dramani Mahama kuwa mjumbe maalumu wa ngazi ya juu wa umoja huo nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2021 07:58 UTC
  • AU yamteua rais wa zamani wa Ghana kuwa mjumbe wake Somalia

Umoja wa Afrika umemteua aliyekuwa rais wa Ghana, John Dramani Mahama kuwa mjumbe maalumu wa ngazi ya juu wa umoja huo nchini Somalia.

Hayo yametangazwa na Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambaye ameeleza kuwa, katika kutekeleza majukumu yake, Mahama atashirikiana na wadau wa Somalia pamoja na Kikosi cha Kulinda Amani cha AU nchini Somalia (AMISOM) kuhakikisha kuwa jitihada za upatanishi na amani zinakwenda sambamba.

Amesema mjumbe huyo maalumu wa AU ametwikwa jukumu la kuzileta pamoja pande hasimu za Somalia katika meza ya mazungumzo na kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika haraka iwezekanavyo.

Mahamat amezitaka pande hasimu nchini Somalia kwenda katika meza ya mazungumzo zikiwa na irada njema ya kisiasa ili kuhakikisha kuwa nchi hiyo inafungua ukurasa mpya wa kidemokrasia. Dramani Mahama alikuwa rais wa Ghana kuanzia tarehe 24 Julai mwaka 2012 hadi Januari 7 mwaka 2017.

Rais wa Somalia aliyemaliza muda wake

Hivi karibuni Umoja wa Afrika ulipongeza hatua ya Bunge la Somalia ya kubatilisha uamuzi wake wa awali wa kumuongezea muda wa uongozi kwa miaka miwili Rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo. 

Rais Mohammad Abdullahi Mohammed wa Somalia alitangaza kuwa, hataongeza muhula wake madarakani kwa muda wa miaka miwili katika kile kilichoonekana kuwa ni kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya kitaifa na kimataifa.

Muhula wake ulimalizika Februari lakini bunge la nchi hiyo hivi karibuni lilimpa idhini ya kutawala kwa miaka mingine miwili, baada ya kukosekana mwafaka wa kufanyika uchaguzi. Hata hivyo baraza la seneti lilipinga uamuzi huo na hivyo kuibua mgogoro mkubwa wa kisiasa.