UN yaitaka serikali ya Gambia iwaachilie huru waandamanaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7018-un_yaitaka_serikali_ya_gambia_iwaachilie_huru_waandamanaji
Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeitaka serikali ya Gambia iwaachilie huru watu waliowekwa kizuizini kwa kushiriki kwenye maandamano ya amani yaliyofanyika Aprili 14 na 16 mwaka huu katika mji mkuu wa nchi hiyo Banjul.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2016 23:21 UTC
  • UN yaitaka serikali ya Gambia iwaachilie huru waandamanaji

Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeitaka serikali ya Gambia iwaachilie huru watu waliowekwa kizuizini kwa kushiriki kwenye maandamano ya amani yaliyofanyika Aprili 14 na 16 mwaka huu katika mji mkuu wa nchi hiyo Banjul.

Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, amesema ofisi hiyo ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya makumi ya waandamanaji waliotiwa nguvuni kwa sababu tu ya kutumia haki yao ya uhuru wa kujieleza, kutoa maoni na kukusanyika.

Colville amebainisha kuwa wamepokea ripoti za kutia wasiwasi zinazoeleza kwamba baadhi ya watu ambao wangali wako kizuizini wameteswa.

Msemaji wa OHCHR amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva kuwa kuna ripoti pia kwamba jamaa wa familia za watu hao wamezuiliwa kuwaona mahabusu hao na baadhi yao wamenyimwa kupatiwa huduma za matibabu.

Fatoumata Jawara na Nogoi Njai, wanasiasa wanawake wa mrengo wa upinzani ambao walihofiwa kuwa wamefariki dunia wamepatikana kizuizini lakini wameripotiwa kuwa wako katika hali mbaya sana.../