May 14, 2016 06:44 UTC
  • Rais Paul Kagame akanusha nchi yake kuwasaidia waasi wa Burundi

Rais Paul Kagame wa Rwanda amekanusha nchi yake kuwasaidia waasi wa Burundi kama ilivyokuja katika ripoti ya siri iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Kagame amesisitiza kuwa, nchi yake haiwasaidii kwa namna yoyote ile waasi wa Burundi au kuhusika na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo jirani. Rais Kagame amebainisha kwamba, machafuko ya ndani nchini Burundi chimbuko lake ni masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Rais wa Rwanda amewaasa walioandaa ripoti hiyo akiwataka kutotoa ripoti ambazo hazisaidii chochote bighairi ya kuleta hali ya kutoelewana baina ya nchi hizo jirani.

Ikumbukwe kuwa, ripoti ya siri iliyowasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, Rwanda inaendelea kuwasaidia waasi wa Burundi wanaotaka kumng'oa madarakani Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa inaituhumu Rwanda kwamba, imekuwa ikitoa mafunzo, misaada ya fedha na ya kilojistiki kwa waasi hao.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni pia Lambert Mende Omalanga msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliituhumu serikali ya Rwanda kuwa inawasaidia kifedha wanachama wa kundi la waasi la M23 waliobaidishiwa katika nchi za Rwanda na Uganda.

Tags