Makumi watoweka baada ya boti kuzama mtoni nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i70592-makumi_watoweka_baada_ya_boti_kuzama_mtoni_nchini_nigeria
Makumi ya watu hawajulikana waliko baada ya boti iliyokuwa imejaza abiria kupindukia kuzama katika mto mmoja huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 27, 2021 02:55 UTC
  • Makumi watoweka baada ya boti kuzama mtoni nchini Nigeria

Makumi ya watu hawajulikana waliko baada ya boti iliyokuwa imejaza abiria kupindukia kuzama katika mto mmoja huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Abdullahi Buhari Wara, afisa mkuu wa utawala katika wilaya ya Ngaski amesema boti hiyo iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 160 ilikatika mara mbili kabla ya kuzama katika Mto Niger katika jimbo la Kebbi la katikati mwa nchi jana Jumatano.

Amesema shughuli ya uokozi inaendelea na kwamba hadi sasa ni watu 22 tu walioweza kuokolewa baada ya kujiri ajali hiyo, huku mwili mmoja ukiopolewa majini. Amesema watu 140 wametoweka kufuatia ajali hiyo.

Afisa huyo wa serikali amesema chanzo cha ajali hiyo ni boti hiyo kubeba watu kupita kiasi, kwani chombo hicho kilipaswa kubeba abiria 80 pekee.

Kujaza abiria kupindukia, moja ya sababu za ajali nyingi za boti baharini na mitoni

Wara amesema mbali na kubeba abiria kupita kiasi, boti hiyo pia ilikuwa imebeba magunia ya mchanga kutoka kwenye timbo moja la dhahabu.

Mapema mwezi huu, watu wasiopungua 30 walikufa maji baada ya boti iliyokuwa imewabeba kupinduka katika jimbo hilo la Niger, la katikati mwa Nigeria.