Somalia kuitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi miwili ijayo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i70632-somalia_kuitisha_uchaguzi_katika_kipindi_cha_miezi_miwili_ijayo
Serikali ya Somalia imetangaza kuwa sasa uchaguzi mkuu uliokuwa umeakhirishwa kwa miezi kadhaa, utafanyika katika kipindi cha siku 60 zijazo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 28, 2021 02:35 UTC
  • Somalia kuitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi miwili ijayo

Serikali ya Somalia imetangaza kuwa sasa uchaguzi mkuu uliokuwa umeakhirishwa kwa miezi kadhaa, utafanyika katika kipindi cha siku 60 zijazo.

Naibu Waziri wa Habari wa Somalia, Abdirahman Yusuf alitangaza habari hiyo jana na kuongeza kuwa, baada ya baraza la ushauri la taifa kukaa na kujadili tarehe ya uchaguzi, sasa imeamuliwa uchaguzi huo ufanyike katika kipindi cha siku 60 zijazo. 

Serikali Kuu na viongozi wa majimbo matano ya Somalia walishindwa kukubaliana kuhusu masharti ya upigaji kura, mivutano ambayo iliendelea hadi muda wa kufanyika uchaguzi yaani mwezi Februari mwaka huu, ukapita na Rais Mohamed Abdullahi Mohamed maarufu kwa jina la Farmajo akaongezewa muda wa urais wake kwa miaka miwili na Bunge la nchi hiyo.

Rais Farmajo wa Somalia

 

Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei, wabunge wa Somalia walipiga kura na kubatilisha uamuzi wao wa awali wa kumuongezea muda wa kubakia madarakani rais huyo.  Bunge la Somalia lilichukua hatua hiyo baada ya kuzuka mivutano na mzozo mkubwa nchini humo.

Baada ya kuongezeka mashinikizo, Rais Farmajo alitangaza kuwa, hataongeza muhula wake madarakani kwa muda wa miaka miwili. Hatua hiyo ilihesabiwa kuwa ni kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya kitaifa na kimataifa.

Baada ya hatua hiyo, Umoja wa Afrika AU ulilipongeza Bunge la Somalia kwa kubatilisha uamuzi wake wa awali wa kumuongezea muda wa uongozi kwa miaka miwili Rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo.

Aidha Umoja wa Afrika ulisifu hatua ya Rais wa Somalia ya kutanguliza mbele maslahi ya taifa hilo na sisitizo lake la kufanyika uchaguzi haraka.