Mjumbe wa UN Somalia apongeza mapatano ya viongozi kuhusu uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i70654-mjumbe_wa_un_somalia_apongeza_mapatano_ya_viongozi_kuhusu_uchaguzi
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia James Swan amepongeza uamuzi uliofikiwa na viongozi wa Somalia wa kufanya uchaguzi wa Rais na Bunge ndani ya miezi miwili, ikiwa ni baada ya siku nne za mazungumzo ya kina yaliyofanyika mjini Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2021 22:21 UTC
  • Mjumbe wa UN Somalia apongeza mapatano ya viongozi kuhusu uchaguzi

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia James Swan amepongeza uamuzi uliofikiwa na viongozi wa Somalia wa kufanya uchaguzi wa Rais na Bunge ndani ya miezi miwili, ikiwa ni baada ya siku nne za mazungumzo ya kina yaliyofanyika mjini Mogadishu.

Swan amewataka viongozi wa serikali kuu ya Somalia na wa serikali za mikoa kuendelea na mawasiliano ya mara kwa mara wakati wote wa mchakato wa uchaguzi ili kuhakikisha kuwa, mvutano wowote unaojitokeza unasuluhishwa haraka.

Jana, Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble na viongozi wa mikoa mitano, pamoja na gavana wa mkoa wa utawala maalumu wa Banadir, walikubaliana kuwa mchakato wa uchaguzi wa Rais na Bunge utamalizika ndani ya miezi miwili.

Naye Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Somalia Mohamed Abdirizak ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa serikali ya Mogadishu imefikia makubaliano na tawala za majimbo ili hatimaye kuwezesha uchaguzi wa kitaifa uliochelewa kufanyika.

Rais Mohamed Abdullahi “Farmajo” wa Somalia

Tarehe ya uchaguzi wa Rais na Bunge itaamuliwa na Bodi ya Uchaguzi, na mchakato mzima utasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Mohamed Hussein Roble.

Hali ya kisiasa nchini Somalia, imekuwa ya taharuki tangu kutibuka kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Februari kutokana na mzozo baina ya makundi ya kisiasa nchini humo.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukimshinikiza Rais Mohamed Abdullahi “Farmajo” kuitisha mazungumzo kati ya serikali yake na tawala za majimbo ili kukubaliana juu ya utaratibu wa kuandaa uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo.