UN: Waasi wa ADF waua raia 57 mkoani Ituri, Congo DR
Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa waasi wa kundi la ADF tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu waliwauwa raia 57 katika kambi za watu wasio na makazi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mashambulizi hayo ya kikatili yaliyofanywa na kundi la waasi wa ADF ambalo katika miaka ya 90 lilifurushwa huko Uganda, yamewalazimisha raia 5,800 kuzikimbia kambi hizo za raia wasio na makazi huko mkoani Ituri mashariki mwa Kongo.
Babar Baloch Msemaji Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amewaambia waandishi wa habari katika ofisi ya shirika hilo huko Geneva Uswisi kwamba, tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu kundi la waasi wa ADF lilifanya mashambulizi mfululizo dhidi ya maeneo ya kambi hizo za watu wasio na makazi katika vijiji vya karibu na miji ya Boga na Tchabi na kuuwa raia 57. Watoto saba ni miongoni mwa watu waliouawa na waasi hao kwa kupigwa risasi na kushambuliwa kwa mapanga.
Raia kadhaa walijeruhiwa katika hujuma hiyo ya waasi wa ADF na watu wengine 25 walitekwa nyara. Waasi hao pia wamechoma moto nyumba na maghala 70 huko Ituri.
Baloch ameeleza kuwa, katika mji wa Boga pekee waasi wa ADF wameuwa watu 31 wakiweno wanawake na watoto wadogo. Ndugu wa familia za wahanga wameeleza kuwa, jamaa zao wengi wamechomwa moto wakiwa hai ndani ya nyumba zao.
Msemaji wa UNHCR amesema shirika hilo limesikitishwa na hujuma mtawalia zinazofanywa na makundi yenye silaha huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Maelfu ya raia wameukimbia mji wa Boga na kuelekea katika maeneo jirani kwa ajili ya usalama wao wakiwa bila ya kitu chochote isipokuwa nguo walizovaa.