UN: Jeshi la DRC liliwasaidia waasi wa Uganda kuua Wakongomani
Ripoti ya siri ya Baraza la Usalama la Umoja wa Matafa imefichua kuwa, kamanda mwandamizi wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alifadhili na kulipa silaha kundi la waasi wa Uganda la ADF kuua raia wa nchi hiyo.
Ripoti hiyo imefichua kuwa, Brigedia Jenerali Muhindo Akili Mundos alilisaidia kundi hilo la waasi wa Uganda kuua raia wa Kongo DR, aliposimamia operesheni iliyopewa jina la Sukola iliyolenga kuzima harakati za waasi hao wa Uganda nchini humo kati ya Agosti mwaka 2014 na Juni mwaka 2015.
Jopo la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa linalosimamia kadhia ya kuwekewa vikwazo DRC limesema kuhusiana na ripoti hiyo kuwa: "Ni wazi sasa kuwa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lilihusika katika kuyafadhili na kuyapa silaha makundi ya waasi kwa lengo la kuua raia wa nchi hiyo."
Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, watu zaidi ya 500 wameuawa katika wimbi la mapigano mashariki mwa Kongo tangu Oktoba mwaka 2014.
Hii ni katika hali ambayo, jeshi la DRC kwa kusaidiwa na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, jana Jumamosi lilianzisha opereseheni ya pamoja ya kijeshi ya kupambana na waasi wa Uganda, mashariki mwa nchi hiyo.
Mac Azukayi, kamanda wa opereseheni ijulikanayo kwa jina la "Sokola 1" amesema kuwa, operesheni hiyo mpya ya jeshi la Kongo DR imeanza katika eneo la Eringeti, mjini Beni na lengo lake ni kuwamaliza kabisa waasi wa ADF wa Uganda wanaofanya mauaji mashariki mwa Kongo. Operesheni hiyo imeanza baada ya waasi hao wa Uganda kuua karibu watu 50 katika mkoa wa Ituri wa kaskazini mashariki mwa Kongo na mkoa wa Kivu Kaskazini wa mashariki mwa nchi hiyo.