Makumi wauawa katika shambulio la anga sokoni kaskazini mwa Ethiopia
Makumi ya watu wameuawa katika shambulio la anga dhidi ya soko moja katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Shambulio hilo lilitekelezwa jana Jumatano huko Tagugun katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia. Hadi sasa idadi kamili ya watu waliouawa haijafahamika. Wafanyakazi watatu wa sekta ya tiba ya Ethiopia wameeleza kuwa, jeshi la nchi hiyo linawazuia watoa huduma za tiba kufika katika eneo la tukio. Shambulio hilo la anga limejiri siku mbili baada ya kutolewa ripoti kuhusu kuanza tena vita huko Tigray.
Mapigano kati ya serikali kuu ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Eneo la Tigray yalianza mwezi Septemba mwaka jana baada ya viongozi wa eneo hilo kuendesha uchaguzi kinyume na agizo la Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed. Abiy Ahmed anaona kuwa, serikali ya eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo iko kinyume cha sheria hivi sasa na inafanya juhudi kulidhibiti eneo hilo kwa nguvu.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa, maelfu ya watu wameuliwa na wengine zaidi ya 950,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao huko Tigray. Hadi sasa raia elfu 50 wa eneo hilo wamewasili Sudan kwa ajili ya hifadhi.