Cyril Ramaphosa asema, machafuko ya Afrika Kusini 'yamechochewa na kupangwa'
(last modified Sat, 17 Jul 2021 03:15:52 GMT )
Jul 17, 2021 03:15 UTC
  • Cyril Ramaphosa asema, machafuko ya Afrika Kusini 'yamechochewa na kupangwa'

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa ghasia kubwa na uporaji ambao umeitikisa nchi hiyo kwa wiki nzima iliyopita vilipangwa na kuchochewa. Ramaphosa ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kwanza katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha baada ya utawala wa ubaguzi wa rangi, Apartheid.

"Ni wazi kabisa kwamba matukio haya yote ya machafuko na uporaji yalichochewa, kuna watu ambao wamepanga na kuratibu matukio haya", amesisitiza Rais wa Afrika Kusini.

Ramaphosa aliyasema hayo jana Ijumaa alipotembelea Manispaa ya Ethikwini, ambayo inajumuisha jiji la bandari la Durban katika mkoa wa KwaZulu-Natal, moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na machafuko, uharibifu na uporaji wa mali.

Amesema serikali yake itawasaka wahusika wakuu wa machafuko hayo ambao baadhi yao tayari wametambuliwa na kwamba, hawatakubali machafuko na ghasia kutokea katika nchi hiyo.

Serikali ya Afrika Kusini ilitangaza siku ya Alhamisi kwamba, mmoja wa watuhumiwa wa uchochezi wa machafuko hayo amekamatwa, na wengine 11 wako chini ya uangalizi. Kwa jumla, watu 2,203 wamekamatwa nchini humo kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizi.

Rais wa Afrika Kusini pia amekiri kwamba, serikali yake ingeweza kuchukua hatua haraka zaidi kuzuia machafuko na kuelezea wasiwasi wake juu ya ongezeko la mivutano ya kikaumu huko KwaZulu-Natal.

Machafuko ya Afrika Kusini

Cyril Ramaphosa pia ameidhinisha kumiminwa mitaani wanajeshi 25,000 ili kudhibiti ghasia zilizozuka nchini humo baada ya kufungwa jela rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma.

Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kuwa, idadi ya watu waliouawa katika ghasia zinazoendelea nchini humo imepindukia 117.

Wiki iliyopita Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini iliagiza Rais mstaafu wa nchi hiyo, Jacob Zuma afungwe jela kwa kukataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi uliofanyika wakati wa uongozi wake kuanzia mwaka 2009 hadi 2018.