Waziri Mkuu wa zamani wa Mali akamatwa kwa madai ya ufisadi
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Mali, Boubeye Maiga ametiwa mbaroni na maafisa usalama wa nchi hiyo, akituhumiwa kuhusika na ufisadi mkubwa wa kifedha.
Wakili wa Maiga, Kassoum Tapo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, sababu za kukamatwa mteja wake haziko wazi, lakini anahusishwa na kashfa ya ununuzi wa ndege ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita.
Tapo amebainisha kuwa, "hatujaona faili la kesi, kwa sasa hatuwezi kutoa maelezo zaidi hadi tulione faili lenyewe."
Ununuzi wa ndege hiyo ya rais wa zamani wa Mali mwaka 2014 kwa thamani ya dola milioni 40 ililalamikiwa vikali na wananchi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi, huku wachumi wakisema ununuzi huo uligubikwa na ufisadi mkubwa wa kifedha, na kwamba ndege yenyewe ilinunuliwa kwa bei ya juu kupita kiasi.

Haijaweza kubainika ushahidi walionao waendesha mashitaka wa serikali kiasi cha kuamua kufungua faili hilo, na vile vile sababu za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Mali wakati huu, baada ya kupitia miaka yote hiyo.
Wadadisi wa mambo wanasema yumkini Maiga ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Mali baina ya 2017-2019 amekamatwa kwa kuwa angetoa ushindani mkali katika uchaguzi wa rais ambao serikali ya mpito inayoongozwa na Assimi Goita imesema utafanyika mwakani.