Kirusi hatari cha Zika charipotiwa Afrika kwa mara ya kwanza
(last modified Fri, 20 May 2016 16:25:34 GMT )
May 20, 2016 16:25 UTC
  • Kirusi hatari cha Zika charipotiwa Afrika kwa mara ya kwanza

Kirusi hatari cha Zika kimeripotiwa kuibuka barani Afrika kwa mara ya kwanza katika Visiwa vya Cape Verde magharibi mwa bara hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ijumaa hii na Shirika la Afya Duniani, WHO, aina ya kirusi kilichogunduliwa nchini humo ni kile ambacho kinasababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ubongo mdogo nchini Brazil na Amerika ya Latini.

Mkrugenzi wa WHO barani Afrika Matshidisho Moeti amesema, kesi hiyo ya Cape Verde ni ushahidi kuwa kirusi cha Zika sasa kimesambaa hadi nje ya bara la Amerika na kuingia Afrika.

Amesema hivi sasa nchi za Afrika zinapaswa kuchukua tahadhari na kutathmini upya njia za kukabiliana na kirushi hicho ambacho kimeenea miongoni mwa maelfu ya watu Amerika ya Latini. Kirusi cha Zika kuligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 1947 na hakikuhesabiwa kuwa hatari hadi kilipoibuka upya mwaka jana Brazil na kusababisha wanawake walioambukizwa kuzaa watoto wenye ubongo mdogo. Kwa msingi huo wataalamu wanasema kirusi cha Zika kilichoibuka Brazil ni hatari zaidi ya kirusi cha zika kilichogunduliwa Afrika miaka iliyopita.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema tafiti zinazoendelea zimebaini kuwa kirusi hicho sasa sio tu kinasambazwa kupitia mbu bali pia kwa njia ya ngono.

Na zaidi ya hapo, tafiti zimebaini kirusi cha zika kwenye majimaji yaliyoko ndani ya nyumba ya uzazi anamokuwemo mtoto wakati wa ujauzito. Baadhi ya nchi zimewashauri wanawake wasishike mimba ili kuzuia watoto kuzaliwa wakiwa na matatizo ya ubongo.