Sudan yacheza ngoma ya Wazayuni, yatwaa mali za harakati ya Hamas
Serikali ya Sudan imefuata nyayo za utawala katili wa Israel na kuchukua hatua ya kutwaa mali na milki za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.
Shirika la Habari la Reuters liliripoti jana kwamba maafisa wa serikali ya Sudan wametwaa mali na milki za harakati ya Hamas na kuzuia miamala yote ya kibenki ya Hamas, makampuni na watu waofanya kazi kwa maslahi ya harakati hiyo ya mapambano ya ukombozi wa Palestina.
Reuters imedai kuwa, mali na milki za Hamas nchini Sudan ni pamoja na hoteli, nyumba, makampuni, mashamba na duka la fedha.
Hatua hiyo iliyo dhidi ya watu wa Palestina ya serikali ya Sudan imechukuliwa miezi kadhaa baada ya Khartoum kusaini makubaliano ya kuanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel chini ya mashinikizo ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump.
Vyama vingi vya upinzani na wananchi wa Sudan wanapinga vikali makubaliano hayo ambayo wanayataja kuwa ni kusaliti mapambano ya ukombozi wa taifa la Palestina na vilevile kibla cha kwanza cha Waislamu.