Maajenti watano wa Intelijinsia Sudan wauawa katika mapigano na Daesh
Idara ya Intelijinsia ya Sudan imetangaza kuwa maajenti wake watano wameuawa na mmoja kujeruhiwa katika shambulio la kuvizia lililoilenga seli ya kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la Jebra huko Khartoum mji mkuu wa nchi hiyo.
Oparesheni hiyo imepelekea kutiwa nguvuni magaidi wa Daesh 11 ambao ni raia wa nchi mbalimbali. Ajenti wa Idara ya Intelijinsia ya Sudan amejeruhiwa pia katika oparesheni hiyo dhidi ya Daesh. Wakati huo huo idadi kubwa ya magaidi wa Daesh wamefanikiwa kukimbia katika shambulio hilo la kushtukiza dhidi ya seli ya wanachama wa Daesh katika mji mkuu Khartoum.
Mapigano kati ya wanachama wa Daesh na idara ya Intelijinsia ya Sudan yamejiri huku hali ya usalama ya Sudan ikilegalega katika siku za karibuni. Serikali ya Sudan hivi karibuni ilidai kujiri jaribio la mapinduzi nchini humo ambalo hata hivyo lilizimwa.
Wahusika kadhaa wa jaribio la mapinduzi Sudan wametiwa nguvuni. Waziri wa Utamaduni na Habari wa Sudan alithibitisha kuwa, wanajeshi waliokuwa na mfungamano na Rais aliyeng'olewa madarakani nchini humo Omar Hassan al Bashir ndio waliopanga jaribio hilo tajwa la mapinduzi.