Magaidi wanne wa ISIS wauawa nchini Sudan
Shirika la kijasusi la Sudan limetoa taarifa na kusema kuwa, wanachama wanne wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) wameuawa nchini humo.
Taarifa hiyo imesema kuwa, makachero wa Sudan wameendesha operesheni maalumu ya kuwasaka wanachama wa Daesh kusini mwa mji mkuu Khartoum na wamepambana nao na kuua magaidi wanne wa ISIS. Askari mmoja wa kikosi maalumu cha shirika hilo la kijasusi la Sudan amejeruhiwa kwenye mapigano hayo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, maafisa usalama wa Sudan walifunga njia zote za kutoka na kuingia kwenye eneo yalipotokea mapigano hayo huko kusini mwa Khartoum, ili kulinda roho na mali za wananchi.
Sasa hivi vikosi vya kulinda usalama nchini Sudan vimeshadidisha na kuongeza sana operesheni zao dhidi ya magenge ya kigaidi.
Kabla ya tukio hilo, shirika la kijasusi la Sudan lilitangaza habari ya kuzuka mapigano kusini mwa Khartoum na yaliyoua maafisa watano wa shirika hilo la kijasusi na mwengine mmoja kujeruhiwa.
Taarifa hiyo ilisema kuwa, magaidi 11 wa Daesh walitiwa mbaroni kwenye operesheni hiyo, lakini magaidi wengine waliokuwa wamejificha waliwavizia maafisa usalama wa Sudan na kuwapiga risasi.
Hayo yameripotiwa katika hali ambayo hali ya kiusalama nchini Sudan si nzuri hata kidogo. Ni hivi majuzi tu ambapo Serikali ya Mpito ya nchi hiyo ilitangaza habari za kufeli jaribio la mapinduzi ambalo ilisema lilipangwa na wafuasi wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jenerali Omar al Bashir.