Hamdok: Sudan inasumbuliwa na mgogoro mbaya zaidi wa kipindi cha mpito
Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok ameonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na "mgogoro mbaya zaidi" katika kipindi hiki cha serikali ya mpito iliyoundwa baada ya kuondolewa madarakani aliyekuwa mtawala wa muda mrefu wa Sudan, Omar al-Bashir zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Matamshi hayo ya Hamdok yametolewa wakati nchi hiyo ikisumbuliwa na mgawanyiko mkubwa kati ya vikundi vya kisiasa na kijeshi ambavyo vinaongoza serikali ya mpito kwa mujibu wa makubaliano ya kugawana madaraka ya Agosti 2019 kwa lengo la kuongoza nchi kuelekea uchaguzi huru na wa haki.
Waziri Mkuu wa Sudan amesema: Kiini cha mgogoro huu ni kutoweza kufikiwa makubaliano juu ya mradi wa kitaifa kati ya makundi ya wanamapinduzi yanayotaka mabadiliko.
Amesema hali hiyo imesababishwa na mgawanyiko mkubwa kati ya raia na wanajeshi.
Abdallah Hamdok amesema: "Mgogoro mkubwa wa kisiasa unaoisumbua Sudan kwa sasa ndio mbaya na hatari zaidi ambao sio tu unatishia serikali ya mpito, lakini pia unatishia nchi yote kwa ujumla."
Jumamosi ya jana pia maelfu ya waandamanaji walikusanyika mbele ya ikulu ya rais mjini Khartoum, wakitoa wito wa kuvunjwa serikali ya sasa ya nchi hiyo na kuhuishwa mapinduzi ya wananchi.