Kushadidi hali ya mgogoro huko Sudan
Mgogoro nchini Sudan umezidi kuwa mkubwa. Wanajeshi wangali wanashikilia madaraka; na Abdel Fattah al Burhan Kamanda Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo ametangaza kuwa siku kadhaa zijazo atatangaza majina ya Waziri Mkuu Mpya na wajumbe wa Baraza la Uongozi. Hii ni katika hali ambayo wananchi wa Sudan wanaendelea kumiminika mitaani kupinga kuendelea wanajeshi kuiongoza nchi hiyo.
Kuhusiana na suala hilo, Muungano wa Vyama Vya Wafanyakazi nchini Sudan umetaka kuvunjwa baraza la kijeshi na kikosi cha radiamali ya haraka na kuhitimishwa nchini humo udhibiti na uingiliaji wa pande za kieneo na kimataifa zinazopinga irada huru ya Wasudani. Muungano huo umetangaza kuwa hakutakuwa na mazungumzo yoyote na baraza la kijeshi lilillofanya mapinduzi na kwamba yoyote atakayeshiriki katika mazungumzo ya aina hiyo haungwi mkono na wananchi.
Maandamano ya wananchi huko Sudan yamepamba moto. Wafanya maandamano hao wanapinga wanajeshi kuendelea kuwepo madarakani na kuamini kuwa hatua hiyo ni mapinduzi ambayo yamevuruga mchakato wa kukabidhi madaraka kwa njia ya kidemokrasia nchini humo. Hii ni katika hali ambayo vitendo vya askari kuwashambulia waandamanaji na kukabiliana nao kwa mabavu vimeongezeka huko Sudan. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa waandamanaji zaidi ya saba wameuawa tangu kujiri mapinduzi nchini. Madaktari wanaotetea demokrasia pia wametangaza kuwa wafanya maandamano wengi wamenyunyiziwa gesi ya kutoa machozi na kulengwa kwa silaha za plastiki.
Wanajeshi wanaotawala Sudan wamewatia hofu wananchi katika kalibu ya senario iliyoratibiwa mapema kwa madai ya kushindwa mapinduzi yaliyopita; na kwa utaratibu huo wameandaa mapinduzi ya karibuni katika kukaribia kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia nchini. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa katiba ya Sudan na mapatano yaliyofikiwa huko nyuma; ilikuwa umesalia chini ya mwezi mmoja tu kabla ya Baraza la Utawala linaloendesha Sudan kukabidhi madaraka kwa viongozi wa kiraia.
Mariam Sadiq al Mahdi Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amesema kuhusu suala hilo kuwa: "Kile kilichotokea Sudan ni mapinduzi dhidi ya makundi ya kiraia na mchakato wa kukabidhi madaraka kwa njia ya kidemkorasia."
Volker Peretz Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya upitishaji kipindi cha mpito huko Sudan ameeleza wasiwasi wake na kuyataja mapinduzi ya karibuni nchini humo kuwa yenye lengo la kudhoofisha kipindi cha mpito cha kisiasa nchini. Wakati huo huo amekutaja kutiwa nguvuni Waziri Mkuu na viongozi wengine wa serikali na wa kisiasa wa nchi hiyo kuwa jambo lisilokubalika.
Sudan inakabiliwa na hali ya mgogoro hivi sasa. Vyama na wananchi wana wasiwasi na utawala wa wanajeshi na kurejea zama za udikteta nchini humo.
Wananchi wa Sudan ambao mwaka 2019 walimiminika kwa wingi mitaani dhidi ya utawala wa kidikteta na kulalamikia hali ngumu ya kiuchumi nchini humo hivi sasa hawahisi kuwepo mabadiliko yoyote nchini mwao baada ya kupita miaka miwili. Kupanda kwa gharama za maisha, umaskini na ukosefu wa ajira yote hayo yanaendelea kuwa matatizo makubwa yanayoitesa Sudan. Katika upande wa kisiasa pia, hatua kama za kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Kizayuni na kutekelezwa juhudi za kuhuisha uhusiano kati ya nchi hiyo na Marekani zimewakasirisha sana wanamapinduzi na vyama mbalimbali nchini humo. Katika upande mwingine, mgogoro wa sasa huko Sudan umezipelekea nchi mbalimbali ajinabi kuingilia zaidi na zaidi masuala ya nchi hiyo. Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ni nchi mbili kuu katika uga wa siasa za Sudan pamoja na utawala wa Kizayuni zinazomuunga mkono jenerali al Burhan. Hata kama Marekani nayo imelaani mapinduzi ya karibuni huko Sudan lakini ina mkono nyuma ya pazia katika matukio ya nchi hiyo; kama ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Washington ilikuwa na taarifa kuhusu suala zima la mapinduzi masaa 48 kabla ya kutokea mapinduzi hayo.
Saleh al Naami mchambuzi wa masuala ya kisiasa ameashiria uwezekano wa Israel kuhusika katika mapinduzi ya wanajeshi huko Sudan na kueleza kuwa: Israel inataka kuzika mageuzi ya kidemokrasia katika Ulimwengu wa Kiarabu, na serikali dhalimu ipo kwa maslahi ya utawala huo.
Muungano wa wafanyakazi nchini Sudan ambao ni taasisi athiri katika siasa nchini humo umepinga pendekezo la kufanya mazungumzo na wanajeshi walioko madarakani; huku makundi ya kisiasa pia yakitaka kuhitimishwa utawala wa wanajeshi nchini humo. Pamoja na hayo, inaonekana kuwa kuendelea hali hiyo imma kutawasha moto wa vita vya ndani nchini humo au utawala wa kijeshi utashuhudiwa kwa mara nyingine tena huko Sudan kwa kusambazwa wanajeshi nchini.