Wanaharakati Sudan watangaza migomo, wakataa pendekezo la kugawana madaraka na jeshi
(last modified Sun, 07 Nov 2021 12:07:08 GMT )
Nov 07, 2021 12:07 UTC
  • Wanaharakati Sudan watangaza migomo, wakataa pendekezo la kugawana madaraka na jeshi

Harakati inayoongoza maandamano ya upinzani nchini Sudan imetangaza migomo ya nchi nzima kwa muda wa siku mbili sambamba na kupinga juhudi zinazoungwa mkono kimataifa za kurejesha utaratibu wa kugawana madaraka na jeshi kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo mwishoni mwa mwezi uliopita.

Jumuiya ya Wasomi Wataalamu wa Sudan (SPA) iliyoongoza vuguvugu la umma lililopelekea kung'olewa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashir imesema juhudi za upatanishi zinazolenga kuleta makubaliano mapya kati ya jeshi na viongozi wa kiraia zitarejesha tena mgogoro, ambao utakuwa ni mbaya zaidi nchini humo.

 Asasi hiyo imetoa mwito wa kufanyika migomo na uasi wa kiraia leo na kesho kwa kutumia kaulimbiu ya "hakuna mazungumzo, hakuna mwafaka, hakuna mgawano wa madaraka" na kuahidi kuendeleza maandamano ya upinzani hadi itakapoundwa serikali ya kiraia kuongoza kipindi cha mpito kuelekea utawala kamili wa kiraia nchini humo.

Mashirika ya habari yameripoti kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum kwamba jumuiya ya SPA iliwataka wananchi waweke vizuizi usiku wa kuamkia leo katika viunga vya mji huo na katika njia kuu ili kuwahamasisha watu na vilevile kupunguza idadi ya watu watakaoelekea makazini leo na kesho.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Abdalla Hamdok

Wananchi wanaounga mkono demokrasia wamekuwa wakifanya maandamano makubwa nchini Sudan kulaani mapinduzi hayo ya kijeshi ambayo yameukengeusha mchakato unaosuasua wa kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia.

Viongozi wa maandamano ya upinzani wamekuwa wakisisitiza msimamo wao wa kutaka wanajeshi wanaoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan wajiweke nje ya ulingo wa siasa.

Tarehe 25 Oktoba, jeshi la Sudan lilifanya mapinduzi kwa kuwakamata wanasiasa wa juu wa kiraia na kuwekwa kwenye kizuizi cha jeshi sambamba na kumweka kwenye kizuizi cha nyumbani Waziri Mkuu Abdalla Hamdok.

Jeshi limekuwa likidhibiti madaraka nchini Sudan katika kipindi kirefu cha historia ya nchi hiyo tangu ilipojipatia uhuru wake mwaka 1956.../

 

 

Tags