Jeshi la Somalia laangamiza magaidi 9 wa al-Shabaab kusini mwa nchi
Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) limetangaza kuwa limeua magaidi tisa wa kundi la al-Shabaab katika wilaya ya Awdhigle kusini mwa nchi hiyo.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumatano, jeshi hilo la Somalia limesema kuwa, magaidi hao al-Shabaab wameuawa katika operesheni ya kiusalama iliyolenga maficho ya genge hilo katika vijiji vya Shamgare na Raqeyle, jimboni Lower Shabelle, kusini mwa nchi.
Wakati huo huo, jeshi la Somalia limefanikiwa kudhibiti msitu wa Kabis ulioko katika jimbo la Gedo katika operesheni inayoendelea ya kiusalama. Wanachama wa al-Shabaab wamekuwa wakiutumia msitu huo kama maficho yao kwa muda sasa.
Wiki iliyopita, jeshi hilo la Somalia lilisema kuwa limefanya operesheni kali katika kijiji cha Gorsarow karibu na mji wa Bulamarer katika jimbo hilo la Lower Shabella na kufanikiwa kuua magaidi wawili ambao walikuwa wanatega mabomu pembeni mwa barabara.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.