5 wauawa katika maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi nchini Sudan
Kwa akali watu watano wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi nchini Sudan.
Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan imesema katika taarifa yake ya jana Jumamosi kuwa, waandamanaji wanne wameuawa kwa kupigwa risasi, huku mmoja akiuawa kwa bomu la gesi ya kutoa machozi katika mji mkuu Khartoum.
Taarifa hiyo imesema, vijana wa miaka 18 na 35 ni miongoni mwa watu waliouawa katika maandamano hayo; na kwamba maafisa usalama wamevamia hospitali moja katika mji wa Omdurman na kuwatia mbaroni majeruhi waliokuwa wakitibiwa hospitalini hapo.
Wananchi wa Sudan walianzisha maandamano mapya usiku wa kumkia jana wakilalamikia mapinduzi ya kijeshi ya nchi hiyo na hatua ya Jenerali Abdul-Fatah al-Burhan ya kuunda Baraza la Utawala.
Maandamano hayo yanayofanyika katika miji mbalimbali ya Sudan kama vile Khartoum, Bahri na Omdurman yametoa wito wa kuhitimishwa utawala wa kijeshi na badala yake kuundwa utawala wa kiraia.
Jenerali Abdul Fatah al-Burhan, kiongozi mkuu wa mapinduzi ya Oktoba 25, alitangaza Baraza jipya la Utawala Alkhamisi ya Novemba 11. Viongozi kadhaa ambao walidai madaraka kukabidhiwa kwa raia, hawakushirikishwa katika baraza hilo.