Askari wasiopungua sita wa Sudan wauawa katika mapigano ya mpakani na Ethiopia
(last modified Sun, 28 Nov 2021 03:35:00 GMT )
Nov 28, 2021 03:35 UTC
  • Askari wasiopungua sita wa Sudan wauawa katika mapigano ya mpakani na Ethiopia

Jeshi la Sudan limesema, askari wake kadhaa wameuawa katika shambulio lililofanywa na vikosi vya jeshi la Ethiopia katika eneo la mpakani linalozozaniwa na nchi mbili.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la Sudan imeeleza kwamba, askari wake waliokuwa wakisimamia zoezi la uvunaji mazao katika eneo la Al-Shafaqa walishambuliwa na makundi ya askari wa jeshi la Ethiopia na wanamgambo waliotaka kuwatisha wakulima na kuvuruga msimu wa mavuno.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, askari wa jeshi la Sudan walijibu shambulio hilo na kusababisha hasara kubwa ya vifo na zana za kijeshi dhidi ya Ethiopia, lakini bila kutaja idadi, ikaongezea pia kwamba, shambulio la jeshi la Ethiopia limepelekea kuuawa askari kadhaa wa Sudan. Ethiopia haijatoa maelezo yoyote juu ya kadhia hiyo.

Hata hivyo vyombo vya habari vimezinukuu duru za jeshi la Sudan zikiripoti kuwa wanajeshi wake wasiopungua sita wameuawa katika mapigano hayo.

Eneo la mpakani la Al-Fashaqa limekuwa likitumiwa na wakulima wa Ethiopia kwa muda mrefu lakini Sudan inadai kuwa ni milki yake.

Eneo hilo ambalo liko kwenye mpaka wa pamoja pia wa ardhi kuu ya Ethiopia na eneo lenye machafuko la Tigray limekuwa likishuhudia mapigano ya hapa na pale ya umwagaji damu kati ya Sudan na Ethiopia kwa miaka kadhaa, lakini makabiliano hayo yalishtadi kuanzia mwaka jana.

Vuta nikuvuta kati ya nchi mbili ziliibuka baada ya mapigano yaliyotokea Novemba 2020 huko Tigray na kusababisha makumi ya maelfu ya wakimbizi kukimbilia Sudan.../

Tags