Radiamali ya Guterres kuhusu kupinga Wasudani kuwepo wanajeshi madarakani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewataka Wasudani kuwa na busara na kuafiki mapatano yaliyosainiwa kati ya Waziri Mkuu na jeshi la nchi hiyo kwa lengo la kudhamini kipindi cha amani cha mpito kuelekea kuundwa serikali ya kiraia huko Sudan.
Guterres amesema kuwa, anafahamu vyema jibu linalotolewa na wale wanaosema "hawataki njia yoyote ya ufumbuzi wa jeshi" lakini amesema kwa mtazamo wake kitendo cha kumrejesha madarakani Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ni ushindi muhimu."
Guterres amesema hivi na hapa ninamnukuu "sisi tuko katika hali isiyoridhisha lakini upo uwezekano wa kuandaliwa mazingira ya kupitisha vizuri kipindi cha mpito kuelekea uundaji wa serikali ya kiraia huko Sudan."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaonya wale wote wanaopinga mapatano ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya Abdallah Hamdok na jeshi na kuendeleza maandamano huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Amesema licha ya kutambua hasira na ghadhabu walizonazo wananchi wa Sudan lakini hakuna shaka kwamba njia ya ufumbuzi kama hiyo itakuwa ya hatari sana kwa Sudan.
Ameongeza kuwa anatoa wito kwa vyama na wananchi wa Sudan kuunga mkono hatua zinazofuata za Waziri Mkuu Abdallah Hamdok kwa ajili ya kukamilisha kipindi cha mpito nchini humo.
Antonio Guterres amebainisha hayo siku moja baada ya maelfu ya wananchi wa Sudan kuandamana karibu wa ikulu ya Rais mjini Khartoum sambamba na kutolewa wito wa kutekelezwa utawala wa kiraia nchini humo. Katika maandamano hayo askari usalama walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Maandamano yanaendelea huko Sudan tangu Mkuu wa jeshi la nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al Burhan aongoze mapinduzi tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka huu na kuvunja taasisi zote za kiutawala za serikali ya mpito sambamba na kuwafuta kazi washirika wake wasio wanajeshi ambao waligawana nao madaraka kwa mujibu wa mapatano yaliyosainiwa mwaka 2019 huko Sudan.