Dec 18, 2021 12:57 UTC
  • Watu tisa wapoteza maisha kufuatia mlipuko wa kipindupindu DRC

Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu umepelekea watu wasiopungua tisa kupoteza maisha katika jimbo la Haut-Lomami, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Madaktari Wasiokuwa na Mipaka (Médecins Sans Frontières- MSF-), huenda watu wengi zaidi wakafariki dunia kwa kukosa huduma za msingi za afya hasa katika eneo la Mulongo.

MSF imetangaza kuwa, iweka kituo cha matibabu chenye vitanda 30, katika eneo la Kabamba ambako ndio kitovu cha maambukizi ya kipindipindu.

Vituo vingine viwili vya kutibu kipindupindu vimefunguliwa Ngoya na Bukena ili kudhibiti maambukizi. Eneo hilo la Mulongo linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maafisa wa afya pamoja na vifaa vya matibabu.

Maafisa wa afya wamesema kwamba, mlipuko wa sasa wa kipindupindu haujawahai kutokea katika sehemu hiyo ya Mulongo tangu milipuko mikubwa ya mwaka 2017 na 2019.

Mratibu wa shughuli za madaktari wasio na mipaka katika jimbo la Haut Lomami, Clement Shap, ameomba msaada kutoka kwa mashirika mengine, akisema kwamba mahitaji ya sasa kukabiliana na ugonjwa huo hayawezi kutoshelezwa na madaktari hao pekee.

Hayo yanajiri siku kadhaa baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutangaza kuwa, mripuko mpya wa homa ya Ebola uliozuka kwenye jimbo la Kivu ya Kaskazini mnamo mwezi Oktoba ukiwa ni wa pili kwa mwaka 2021, umemalizika.

Tags