Watu milioni 8 wanahitajia msaada wa chakula Malawi
Serikali ya Malawi imesema kuwa, zaidi ya watu milioni 8 wanahitajia msaada wa chakula nchni humo.
Godfrey Chaponda, Waziri wa Kilimo wa nchi hiyo amesema watu milioni 8.4 wanakodolewa macho na baa la njaa lililosababishwa na ukame. Waziri huyo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa nchi hiyo inakabiliwa na ukame kutokana na taathira hasi za mabadiliko ya hali ya hewa yajulikanayo kama el-Nino.
Kauli ya Wizara ya Kilimo ya Malawi imetolewa siku chache baada ya Rais Peter Mutharika wa nchi hiyo kutangaza kuwa nchi yake imo katika janga la kitaifa kufuatia ukame mkubwa ulioikumba nchi hiyo, katika msimu wa mavuno ya kilimo wa mwaka 2015/16.
Taarifa ya Rais wa Malawi ilieleza kuwa, kupungua kwa mavuno ya zao la mahindi kunakadiriwa kuwa asilimia 12 kulingana na mavuno ya mwaka uliopita. Alisema watu wengi watakabiliwa na tatizo la chakula na watahitajia msaada wa kibinadamu katika kipindi cha mwaka 2016/17. Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) umesema kuwa tayari unawasaidia wananchi wa Malawi karibu milioni tatu wanaokabiliwa na tatizo la chakula.