Wanawake nchini Sudan waandamana, wapinga kubakwa waandamanaji wa kike
(last modified Fri, 24 Dec 2021 15:52:40 GMT )
Dec 24, 2021 15:52 UTC
  • Wanawake nchini Sudan waandamana, wapinga kubakwa waandamanaji wa kike

Hali ya taharuki imetanda katika duru za Sudan kwa siku kadhaa sasa, huku habari zikisambaa kuwa idadi kubwa ya vijana wa kike walibakwa na kunyanyaswa walipokuwa wakishiriki maandamano Jumapili iliyopita dhidi ya utawala wa kijeshi.

Duru za haki za binadamu na vyombo vya habari zinawashutumu wanachama wa vikosi vya jeshi la Sudan kuwa wamehusika katika ubakaji wa wasichana wanaoshiriki maandamo dhidi ya utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

Miji ya Sudan imekumbwa na maandamano ya mara kwa mara tangu Oktoba 25 kupinga maamuzi ya Kamanda Mkuu wa Jeshi, Abdel Fattah Al-Burhan, ambaye alisimamisha hati ya katiba, kutangaza hali ya hatari na kuiondoa madarakani serikali ya kipindi cha mpito.

Maamuzi hayo ya al Burhan yalisababisha maandamano na machafuko makubwa ya raia, asasi za kijamii na vyama vya siasa vilivyoamua kupaza sauti ya kuwataka wanajeshi wajitoe kwenye siasa na kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Maandamano hayo ya wananchi wa Sudan yanaendelea, licha ya jeshi kumrejesha madarakani Waziri Mkuu, Abdullah Hamdok.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na duru za matibabu zinalamu matumizi ya mabomu ya machozi ambayo yanaathiri mfumo wa fahamu na upumuaji, na kumekuwapo ripoti za ubakaji wa wasichana walioshiriki maandamano ya tarehe 19 mwezi huu wa Disemba.

Jana, Alhamisi, mashirika, jumuiya na harakati 40 za watetezi wa haki za wanawake nchini Sudan ziliitisha maandamano kupinga uhalifu huo na kukabidhi risala kwa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu nchini humo.

Maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi Sudan

Maandamano kama hayo ya kupinga ubakaji unaofanywa na jeshi la Sudan dhidi ya waandamanaji wa kike pia yameshuhudiwa katika miji mingine kadhaa ya Sudan.

Mwandishi wa al Jazeera nchini Sudan, Halah al Karib anasema: "Taasisi ya jeshi imetumia ubakaji kama njia ya kuwadhalilisha wanawake na jamii huko Darfur kwa zaidi ya miaka 20, na uhalifu wa ubakaji uliofanyika Khartoum wakati wa kutawanywa mgomo na maandamano  haukupewa mazingatio wala kufuatiliwa na serikali ya mpito, sawa na mauaji yaliyofanywa katika kutawanya mgomo na maandamano hayo."

Tags