Financial Times latahadharisha: Ash-Shabaab wanaweza kurudi tena madarakani Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78630-financial_times_latahadharisha_ash_shabaab_wanaweza_kurudi_tena_madarakani_somalia
Gazeti la Financial Times limetahadharisha kuwa, kundi la kigaidi la Ash-Shabaab linaweza likarudi upya kwenye medani na kuidhibiti tena Somalia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 30, 2021 11:40 UTC
  • Financial Times latahadharisha: Ash-Shabaab wanaweza kurudi tena madarakani Somalia

Gazeti la Financial Times limetahadharisha kuwa, kundi la kigaidi la Ash-Shabaab linaweza likarudi upya kwenye medani na kuidhibiti tena Somalia.

Katika ripoti kuhusu mapigano mapya yaliyozuka nchini Somalia na kuzidi kupata nguvu kundi la kigaidi la Ash-Shabaab, Financial Times limeandika, kutokana na mivutano ya kikanda inayoendelea ndani ya Sudan na Ethiopia na mizozo ya kisiasa ya ndani, inavyoonekana, kundi hilo linaendelea kurudi kwenye medani kwa nguvu kamili na kuidhibiti tena Somalia.

Kwa mujibu wa ripoti ya Financial Times, hivi sasa mapigano yamefika mji wa Goyal, na kwamba taasisi na hospitali za mji huo zimebomolewa kikamilifu; na huo ni mji ambao ulikuwa kitovu na kimbilio kwa ajili ya kusimamia suluhu, maridhiano na mapatano nchini Somalia.

Kulingana na makadirio na tathmini iliyotolewa na wafanyakazi wa ufikishaji misaada, katika mwaka huu wa 2021, mji wa Goyal umeshuhudia mapigano makubwa zaidi ya umwagaji damu, kiasi kwamba kuanzia mwezi Oktoba hadi sasa mapigano katika mji huo yameua watu 12 na kuwalazimisha wengine zaidi ya 100 kuuhama mji.

Kundi la kigaidi la Ash-Shabaab ambalo lina mfungamano na mtandao wa Al Qaeda lilianzisha hujuma na mashambulio tangu mwaka 2007 kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia.

Mwaka 2011, vikosi vya Umoja wa Afrika AMISOM vikishirikiana na vya jeshi la serikali ya Somalia viliwatimua wanamgambo wa Ash-Shabaab katika mji mkuu Mogadishu, hata hivyo kundi hilo lingali linaendelea kudhibiti sehemu nyingi za maeneo ya vijijini katika nchi hiyo.../