AU yataka pande hasimu za kisiasa Somalia zifanye mazungumzo
Umoja wa Afrika umetoa mwito kwa Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo wa Somalia na Waziri Mkuu wa nchi hiyo aliyesimamishwa kazi hivi karibuni, Mohamed Hussein Roble kufanya mazungumzo haraka iwezekanavyo, baada ya wawili hao kutofautiana vikali wakati huu wa kuendelea uchaguzi wa bunge.
Disemba 27, Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo alitangaza kumsimamisha kazi Waziri Mkuu, Mohamed Hussein Roble akimtuhumu kuwa amehusika na ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma. Roble amekanusha vikali tuhuma hizo.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mousa Faki Mahamat amewaasa viongozi hao wa Somalia kutanguliza mbele maslahi ya taifa na kupunguza mvutano wa kisiasa unaoweza kuitumbukiza nchi hiyo ya Pembe ya Afrika katika hali mbaya zaidi.
Mahamat amewataka viongozi hao kufanya mazungumzo ili kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mzozo uliopo. Kwa muda sasa wanasiasa hao wawili wamekuwa wakizozana kuhusu uchaguzi wa bunge na wamefikia hata kulumbana hadharani.

Mzozo huo mpya wa kisiasa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayosumbuliwa na njaa na hujuma za kigaidi, umeitia wasiwasi mkubwa jamii ya kimataifa.
Hivi karibuni, Jumuiya ya Maendeleo ya Kieneo IGAD, ilisema kuna udharura wa kutekelezwa mara moja makubaliano ya tarehe 17 Septemba 2020 na 27 Mei 2021, ambayo ni msingi wa uchaguzi unaoendelea, ili mchakato wa zoezi hilo umalizike, na matokeo yake yakubaliwe na wananchi wa Somalia.