Umoja wa Afrika na Somalia kutathmini hatima ya AMISOM
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78692-umoja_wa_afrika_na_somalia_kutathmini_hatima_ya_amisom
Somalia na Umoja wa Afrika (AU) zimekubaliana kutathmini operesheni za vikosi vya nchi wanachama wa umoja huo AMISOM, ambavyo muda wake uliongezwa mpaka mwezi Machi mwaka 2022.
(last modified 2026-02-17T17:08:55+00:00 )
Jan 01, 2022 07:56 UTC
  • Umoja wa Afrika na Somalia kutathmini hatima ya AMISOM

Somalia na Umoja wa Afrika (AU) zimekubaliana kutathmini operesheni za vikosi vya nchi wanachama wa umoja huo AMISOM, ambavyo muda wake uliongezwa mpaka mwezi Machi mwaka 2022.

Katika kikao cha pamoja kati ya serikali ya Somalia na wawakilishi wa Umoja wa Afrika, pande hizo mbili zimekubaliana kuanza majadiliano kuhusu hatima ya vikosi vya AMISOM, kuanzia Januari, majadiliano ambayo yanatarajiwa kuendelea kwa muda wa siku 30.

Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa na pande hizo mbili ni pamoja na namna ya kufadhili operesheni hiyo na namna ya kuendeleza mapambano dhidi ya kundi la Al Shabab na makundi mengine ya kigaidi nchini Somalia.

Baada ya majadiliano hayo, serikali ya Mogadishu na AU zinatarajiwa kuwasilisha ripoti yao kwa Tume ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika, kuanzia Februari 11 mwaka huu wa 2022.

Ni wiki iliyopita tu ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliongeza muda wa AMISOM kusalia nchini Somalia kwa kipindi cha miezi mitatu zaidi, wakati huu Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika linapotarajiwa kupendekeza kikosi hicho kusalia nchini humo mpaka 2023.../