Tarehe mpya ya Uchaguzi wa Rais nchini Libya
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya imetangaza tarehe 24 mwezi huu wa Januari 2022 kuwa siku ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo licha ya kwamba bado kuna hitilafu kuhusu wakati hasa unaopaswa kufanyika uchaguzi huo.
Kwanza uchaguzi huo wa Libya ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 24 Disemba, mwaka jana 2021 lakini uliakhirishwa kutokana na hitilafu mbalimbali kama za nani wanafaa kugombea na vile vile kutowasilishwa orodha kamili za wagombea. Dk. Imad al-Sayeh, Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya amesema kwamba tume hiyo itatangaza majina yote ya wagombea bila ya kumtuhumu mgombea yeyote na wala kufuta jina llolote. Aidha amesema, tarehe ya uchaguzi huo imesongezwa mbele baada ya tume hiyo kushindwa kupatiwa orodha kamili ya wagombea.
Kuakhirishwa tarehe ya uchguzi wa Libya kumeongeza wasiwasi kuhusu mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo. Baadhi ya makundi ya kisiasa yanaamini kuwa, kuakhirishwa tarehe ya uchaguzi nchini Libya kumezidi kutatanisha juhudi za kufanikisha zoezi hilo, bali kumeongeza uwezekano wa kuanza tena vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Waatu wengi wanaamini kuwa, uchaguzi nchini Libya unapaswa kufanyika katika wakati mwafaka na baada ya kuandaliwa mazingira bora. Vile vile masharti ya kuweza kugombea inabidi yawekwe wazi bila ya utata wowote.
Dk. Ali Muhammad al-Sallabi, mchambuzi wa masuala ya Libya anasema: Maelewano na mshikamano wa kijamii na kisiasa ndio msingi mkuu unaopaswa kuheshimiwa kwanza kabla ya kuchukkuliwa hatua nyingine yoyote ya kisiasa kwani ni kwa njia hiyo ndipo utaweza kupatikana utulivu na umoja wa kitaifa nchini Libya.
Bi Stephanie Williams, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya anasema, wasiwasi mkuu uliojitokeza baada ya kuakhirishwa tarehe ya uchaguzi wa rais wa Libya umo kwenye namna ya kuitishwa uchaguzi huo na hatima ya serikali ya mpito hasa kwa vile Walibya wengi wanataka serikali mpya na hawafurahishwi na kuendelea kutawaliwa na serikali ya mpito.
Mivutano baina ya makundi ya kisiasa nchini Libya inaendelea katika hali ambayo, uingiliaji wa madola ajnabi nao unazidi kuleta mivutano nchini humo. Balozi za nchi za Magharibi za Marekani, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Italia zimetoa tamko la pamoja la kuingilia masuala ya ndani ya Libya zikidai kuwa jamii ya kimataifa iko tayari kuwapandisha kizimbani wanaochochea machafuko na kuvuruga mchakato wa kisiasa na uchaguzi wa Libya.
Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amesema: Libya hivi sasa inavuuka kipindi hatari sana. Kila mmoja ana wajibu wa kusaidia kufanikishwa juhudi za kuivuusha salama Libya katika kipindi hiki kizito na hatari. Kufanyika uchaguzi haraka iwezekanavyo kunaweza kuwasaidia wananchi wa Libya kufanikisha malengo yao ya kulinda umoja na mshakamano wao wa kitaifa.
Hivi sasa imetangazwa tarehe 24 mwezi huu wa Janauri kuwa tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi nchini Libya. Pamoja na hayo bado kuna hitilafu kuhusu tarehe hizo huku matatizo yaliyopelekea kuakhirishwa uchaguzi huo yakiwa bado hayajatatuliwa. Khalid al-Mishri, Mkuu wa Baraza Kuu la Libya amesema kuwa, sababu iliyopelekea ishindikane kuitishwa uchaguzi mwezi Disemba, ni kukosekana msingi mmoja wa kisheria uliokubaliwa na wote. Vilevile amesema: Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya imetangaza tu kiholela tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi huo bila ya kuwa na msingi wowote wa kutegemewa kitaifa na kisheria.
Kwa kuzingatia yote hayo tutaona kuwa, mivutano ya kisiasa nchini Libya bado ni mikubwa. Uingiliaji wa madola ya kigeni kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja pia ni mkubwa; na hayo ndiyo matatizo makuu yanayokwamisha juhudi za kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Libya.