UNICEF: Pande zinazozozana Tigray Ethiopia zimefanya ukandamizaji dhidi ya watoto
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umezituhumu pande zinazopigana katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia kwamba, zimefanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya watoto.
Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) sambamba na kuonyesha hasira zake kwa mashambulio ya hivi karibuni ya anga dhidi ya kambi za wakimbizi katika jimbo la Tigray amesema kuwa, mashambulio hayo tarehe 5 na 7 mwezi huu wa Januari yamesababisha makumi ya watu kuuawa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA imetangaza kuwa, watu 56 wameuawa na wengine 36 kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya anga dhidi ya kambi ya wakimbizi huko Tigray.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa umesitisha operesheni za kupeleka misaada ya kibinadamu katika jimbo la Tigray baada ya ndege za kijeshi za Ethiopia kushambulia kambi ya wakimbizi katika eneo hilo.

Disemba 30 mwaka jana Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliripoti kuwa, makumi ya raia wameuawa katika mashambulizi ya anga kusini mwa eneo la Tigray. Umoja wa Mataifa uliyataja mauaji hayo ya raia kuwa mashambulizi makali zaidi kuwahi kuripotiwa tangu mwezi Oktoba mwaka jana.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, juzi serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwa itatoa msamaha na kuwaachia huru wafungwa mashuhuri wa kisiasa akiwemo kiongozi wa upinzani Jawar Mohammed na maafisa wa chama cha upinzani cha Tigray; hatua ambayo inaandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya kitaifa.