Upinzani Kenya kumshtaki rais kwa tuhuma za ufisadi
Viongozi wa upinzani nchini Kenya wamesema kuwa wanajiandaa kwenda mahakamani kumshtaki Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo na naibu wake William Ruto, kwa kushindwa kuwaeleza wananchi nanmna walivyotumia mkopo wa Eurobond wa shilingi bilioni 253 za Kenya.
Mmoja wa vinara wa muungano wa upinzani wa Cord, Moses Wetangula amesema serikali ya Nairobi imekuwa ikipuuza wito wao wa kulielezea taifa namna pesa hizo zilivyotumika na badala yake wamekuwa wakiwapuuza na kusema kuwa viongozi wa upinzani wanapiga makelele yasiyokuwa na msingi.
Wetangula ambaye pia ni Seneta wa kaunti ya Bungoma magharibi mwa Kenya amesema kuwa, awali Rais Kenyatta na naibu wake Ruto waliwapuuza walipofichua kashfa ya ufisadi ya shilingi milioni 791 katika shirika la huduma kwa vijana NYS. Waziri wa Ugatuzi na Mipango Ann Waiguru ambaye shirika hilo liko chini ya wizara hiyo alijiuzulu kufuatia mashinikizo ya kila upande ya upinzani, ingawa binafsi alisisitiza kuwa alichukua hatua hiyo kutokana na sababu za kiafya.
Kinara huyo wa upizani anahoji kuwa, inakuaje Naibu wa Rais kila mwishoni mwa wiki anatoa shilingi milioni 100 katika hafla za kuchangisha pesa maarufu kama Harambee iwapo sio ufisadi?