IMF kuinyima fedha Somalia iwapo itaakhirisha tena uchaguzi
(last modified 2022-02-23T02:37:46+00:00 )
Feb 23, 2022 02:37 UTC
  • IMF kuinyima fedha Somalia iwapo itaakhirisha tena uchaguzi

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema huenda likasimamisha ushirikiano wake wa kifedha na serikali ya federali ya Somalia katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, iwapo nchi hiyo ya Pembe ya Afrika itaakhirisha tena uchaguzi.

Hayo yalisemwa jana Jumanne na Laura Jaramillo Mayor, Mkuu wa ofisi ya IMF nchini Somalia na kuongeza kuwa, "Mipango ya IMF nchini Somalia itaangalia upya katikati ya Mei, lakini kuendelea kuakhirishwa uchaguzi kuna maana kwamba serikali mpya huenda isiweze kuidhinisha mageuzi mapya kwa wakati mwafaka."

Amesema iwapo IMF itachukua hatua ya kuisimamishia Somalia msaada, basi bajeti ya nchi hiyo maskini ya Kiafrika itaathiriwa pakubwa, na vile vile mpango wa kuipunguzia deni la taifa kutoka dola bilioni 5.2 za Marekani la kuanzia mwaka 2018, hadi dola milioni 557.

Uchaguzi Somalia

Uchaguzi wa Somalia umecheleweshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kutokana na mizozo ya kisiasa, huku ule wa Bunge la Chini la nchi hiyo ukitazamiwa kumalizika Ijumaa ijayo.

Hata hivyo waangalizi wengi wa uchaguzi wanasema kuna uwezekanao mkubwa nchi hiyo ikashindwa kukamilisha zoezi hilo kufikia Ijumaa kama ilivyoratibiwa, kwa kuwa wabunge zaidi ya 100 wa Bunge hilo bado hawajachagulia mpaka sasa. 

 

Tags