Somalia yaakhirisha tena muhula wa kumalizika uchaguzi wa Bunge
Kwa mara nyingine tena, Somalia imetangaza kusogeza mbele muhula wa mwisho uliokuwa umewekwa kwa ajili ya kumalizika uchaguzi wa Bunge nchini humo.
Waziri Mkuu wa Somalia, Mohamed Hussein Roble ametangaza hayo na kuongeza kuwa, zoezi hilo la kuwachagua wabunge wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika sasa litakamilika kufikia Machi 15.
Uchaguzi wa Bunge Somalia ambao umecheleweshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kutokana na mizozo na mivutano ya kisiasa, ulikuwa unatazamiwa kumalizika jana Ijumaa.
Baraza la Mashauri ya Kitaifa la Somalia limesema uchaguzi huo umeakhirishwa mara kadhaa kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiusalama, ukame, na ukosefu wa fedha za misaada.
Hivi karibuni, Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilisema huenda likasimamisha ushirikiano wake wa kifedha na serikali ya federali ya Somalia katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, iwapo nchi hiyo itaakhirisha tena uchaguzi huo.
Zoezi la kuwachagua wabunge wa Somalia pamoja na maseneta 54 lilianza Novemba mwaka jana; wawakilishi ambao wana dhamana ya kumchagua rais mpya wa nchi hiyo. Kufikia sasa, ni wabunge 184 kati ya 275 wa Bunge la Chini ya nchi hiyo waliochaguliwa.