Serikali ya Libya yakomboa eneo jengine muhimu la kiistratijia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8173-serikali_ya_libya_yakomboa_eneo_jengine_muhimu_la_kiistratijia
Vikosi maalumu vya kulinda taasisi za mafuta nchini Libya vimefanikiwa kulikomboa eneo moja la kiistratijia mashariki mwa mji wa bandari wa Sirte wa kaskazini mwa nchi hiyo, kutoka mikono mwa kundi la kigaidi la ISIS yaani Daesh.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 31, 2016 07:49 UTC
  • Serikali ya Libya yakomboa eneo jengine muhimu la kiistratijia

Vikosi maalumu vya kulinda taasisi za mafuta nchini Libya vimefanikiwa kulikomboa eneo moja la kiistratijia mashariki mwa mji wa bandari wa Sirte wa kaskazini mwa nchi hiyo, kutoka mikono mwa kundi la kigaidi la ISIS yaani Daesh.

Msemaji wa vikosi hivyo maalumu amesema kuwa, mji wa Bin Jawwād wa mashariki mwa bandari ya Sirte ambayo ni ngome ya kundi la kigaidi la Daesh, umekombolewa.

Msemaji huyo ameongeza kuwa, askari wanne wa vikosi maalumu vya kulinda taasisi za mafuta nchini Libya wameuawa katika operesheni hiyo na askari 16 wengine wamejeruhiwa.

Vikosi hivyo vimetangaza kuwa vinaiunga mkono serikali mpya ya umoja wa kitaifa.

Hivi sasa vikosi vya ulinzi vya Libya vinafanya juhudi za za kukomboa kinu kimoja cha umeme kilichoko umbali wa kilomita 15 kutoka katikati ya mji wa Sirte.

Makundi mengine ya kijeshi yanayoiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, yanaendelea kusonga mbele kuelekea kwenye viunga vya magharibi mwa mji wa Sirte.

Kundi la Daesh lilitumia mwanya wa kukosekana serikali yenye nguvu nchini Libya, kuuvamia na kuuteka mji wa bandari wa Sirte na kupanua eneo la kilomita 250 la udhibiti wake.