Somalia yakaribisha kuundwa kikosi cha mpito cha Umoja wa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i82046-somalia_yakaribisha_kuundwa_kikosi_cha_mpito_cha_umoja_wa_afrika
Serikali ya Federali ya Somalia imepongeza hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukipangua Kikosi cha Kijeshi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na kuunda kikosi kipya cha amani cha mpito cha ATMIS.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 02, 2022 02:36 UTC
  • Somalia yakaribisha kuundwa kikosi cha mpito cha Umoja wa Afrika

Serikali ya Federali ya Somalia imepongeza hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukipangua Kikosi cha Kijeshi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na kuunda kikosi kipya cha amani cha mpito cha ATMIS.

Kikosi hicho cha mpito cha Umoja wa Afrika (ATMIS) kilianza kazi jana Ijumaa, siku moja baada ya AMISOM kumaliza jukumu lake la kuidhaminia usalama Somalia na kupambana na magenge ya kigaidi kwa miaka 15. ATMIS inatazamiwa kumaliza shughuli zake mwaka 2024.

Serikali ya Somalia imesema imejitolea kwa dhati kuhakikisha kuwa mchakato wa kukabidhiwa jukumu la usalama wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kutoka kikosi hicho kipya cha muda, unafanyika vizuri na ndani ya muda ulioanishwa.

Siku ya Alkhamisi, Baraza la Usalama la UN lilipasisha kwa kishindo azimio nambari 2628 la kuundwa kikosi hicho kipya, na kuiruhusu AU kutuma askari 19,626, wakiwemo maafisa wa polisi 1,040, kufikia Disemba 31, na idadi hiyo ipunguzwe hadi 17,626 baina ya Januari Mosi na Machi 31, 2023.

Baraza la Usalama la UN

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliongeza muda wa AMISOM kusalia nchini Somalia kwa kipindi cha miezi mitatu zaidi, ingawaje Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilipendekeza kikosi hicho kusalia nchini humo mpaka 2023.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukifadhili askari hao wa AMISOM wapatao 21,000, ambao wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007. Wanajeshi wa AMISOM ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone, huku maafisa wa polisi wa kikosi hicho cha AU wakitoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.