Watoto laki 3 kufariki Somalia iwapo misaada haitawafikia haraka
Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa watoto zaidi ya 370,000 watapoteza maisha ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Juni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuwafikishia misaada ya dharura.
Adam Abdelmoula Mratbibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Somali amesema hali ni mbaya sana na kuongeza kuwa watu milioni 7.1 watakumbwa na njaa kali kama oparesheni kubwa ya kutoa misaada ya kibinadamu haitatekelezwa kabla ya mwaka huu kumalizika.
Abdelmoula aliyasmea hayo Jumanne alipokuwa anatembelea mji wa Baidoa nchini Somalia na kusema hali imekuwa mbaya nchini humo kwa sababu ya kutokuwa na mvua katika kipindi cha misimu mitano mfululizo.
Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud pia ametembelea Baidoa ili aweze kutathmini hali ya njaa katika eneo hilo sambamba na kuzindua kampeni ya kitaifa ya kutoa misaada kwa wanaohitaji kote katika nchi hiyo. Ametoa wito kwa nchi wafadhili na Wasomali wenye uwezo kutuma misaada ya haraka ili kuzuia vifo.

Hayo yanajiri wakati ambao mashirika sita ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa masuala ya kibinadamu wiki hii wametoa tahadhari ya baa la njaa kunyemelea eneo la Afrika Mashariki baada ya miaka minne ya ukame mkali huku uhaba wa mvua kwa mwaka mwingine wa tano mfululizo ukitabiriwa.
Taarifa hiyo imesema Somalia na maeneo kadhaa ya Kenya na Ethiopia yameathiriwa na baa la hali mbaya ya ukame ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa miaka 40 sasa, ambapo misimu minne mfululizo ya mvua imekuwa na kiwango cha chini kabisa cha mvua.