Algeria yasimamisha ushirikiano na Uhispania kwa sababu ya kadhia ya Sahara Magharibi
(last modified Thu, 09 Jun 2022 12:25:42 GMT )
Jun 09, 2022 12:25 UTC
  • Algeria yasimamisha ushirikiano na Uhispania kwa sababu ya kadhia ya Sahara Magharibi

Algeria imechukua hatua "mara moja" kusimamisha mkataba wa Urafiki baina yake na Uhispania baada ya Madrid kubadilisha msimamo wa miongo kadhaa wa kutoegemea upande wowote katika mgogoro wa Sahara Magharibi.

Uamuzi huo wa Algeria ni pigo jipya kwa uhusiano unaozidi kulegalega wa Algiers na Madrid, ambayo inaitegemea Algeria kwa ajili ya nishati ya gesi asilia.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Algeria imesema: "Algeria imeamua kusimamisha "mara moja" mkataba wa urafiki, ujirani mwema na ushirikiano iliosaini na Uhispania mwaka 2002.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Uhispania inaharibu nafasi yake ya "mamlaka ya uendeshaji" katika Sahara Magharibi inayopasa kuwa nayo hadi pale Umoja wa Mataifa utakapotatua mgogoro wa miongo kadhaa kuhusu hatima ya eneo hilo lenye utajiri wa madini.

Ofisi ya rais wa Algeria imesisitiza katika taarifa yake kwamba, kwa maana hiyo, inachofanya serikali ya Madrid ni kuchangia moja kwa moja katika kuharibu hali ya Sahara Magharibi na eneo kwa ujumla.

Kwa upande wake, serikali ya Uhispania imesema imesikitishwa na uamuzi wa Algeria na kusisitiza kwamba itaendelea kudumisha mkataba huo wa urafiki.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Uhispania imesema: "Serikali ya Uhispania inaitazama Algeria kama nchi jiraini rafiki na inasisitiza utayarifu wake kamili wa kudumisha na kuendeleza uhusiano maalumu wa ushirikiano baina ya nchi zetu mbili kwa faida ya watu wa pande zote mbili."

Hatua iliyochukuliwa na Algeria imeipa changamoto kali na tata Uhispania ya kuleta uwiyano wa mahusiano yake na Morocco na Algeria, ambayo mwezi Agosti mwaka jana ilichukua uamuzi wa kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Morocco kutokana na kile ilichokiita "hatua za kiuadui" za Rabat.

Kwa sasa, Morocco inadhibitii asilimia 80 ya eneo la Sahara Magharibi huku sehemu iliyosalia ikishikiliwa na Harakati ya Polisario inayoungwa mkono na Algeria. Kwa miaka 15, Polisario imepigana vita na Morocco vya kulikomboa eneo hilo, baada ya Uhispania kuondoa askari wake mwaka 1975 na inataka iitishwe kura ya maoni ya kuamua uhuru na kujitawala watu wa Sahara Magharibi.../